9 Mei 2025 - 22:08
Majlis ya Mazazi ya Imam Ridha (as) yafanyika Jamiat Al-Mustafa(s), Tanzania | Hadithi Toka Vyanzo vya Kisunni Zinathibitisha Makhalifa Kumi na Wawili

Lengo la Mazungumzo Haya ni: Kuleta maelewano baina ya Madhehebu za Kiislamu na kuonyesha kuwa msingi wa Uimamu na Ukhalifa wa Maimam Kumi na Wawili wa Ahlul-Bayt (a.s), wanaofuatwa na Waislamu wa Madhehebu ya Shia Ithna Ashari, una mizizi pia katika vyanzo vinavyokubalika vya Kisunni.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) - ABNA- Katika kuadhimisha Mazazi ya Imam Ali bin Musa al-Ridha (a.s), Jamiat Al-Mustafa (s), Dar es Salaam - Tanzania iliandaa Majlis maalum iliyohudhuriwa na Waumini wa Madhehebu ya Shia Ithna Ashari na wageni mbalimbali. Mzungumzaji katika hafla hiyo alikuwa Sheikh Issah Chande, ambaye Msomi na Mhitimu wa Chuo hicho cha Jamiat Al-Mustafa (s), Dar-es-Salam -Tanzania.

Katika hotuba yake, Sheikh Chande alielezea kwa kina kuhusu ushahidi wa Ukhalifa wa Maimamu Kumi na Wawili (a.s) kutoka katika vyanzo vya Hadithi vya Kisunni. Alisisitiza kuwa hata katika vitabu vya Ahlul-Sunna, kuna ushahidi unaoashiria kuwepo kwa viongozi wa haki na Makhalaifa Kumi na wawili kutoka katika Kizazi Kitukufu cha Mtume wetu Muhammad (saww).

Majlis ya Mazazi ya Imam Ridha (as) yafanyika Jamiat Al-Mustafa(s), Tanzania | Hadithi Toka Vyanzo vya Kisunni Zinathibitisha Makhalifa Kumi na Wawili


🔹 Hadithi ya Maimamu Kumi na Wawili (a.s)

Sheikh Chande alinukuu Hadithi maarufu inayopatikana katika vitabu vya Kisunni kama ifuatavyo:

📖 Sahih Muslim, Juzuu 3, Ukurasa 1452, Hadithi Na. 1821:

"Dini hii itaendelea kuwa imara mpaka Siku ya Kiyama ikiwa chini ya Viongozi kumi na Wawili, wote kutoka kwa Makuraysh."

📖 Musnad Ahmad ibn Hanbal, Juzuu 5, Uk. 89 na 99:

"Kutakuwa na viongozi kumi na wawili, wote kutoka kwa Makuraysh."

📖 Sunan Abi Dawud, Hadithi Na. 4280:

"Uislamu utabaki imara chini ya viongozi kumi na wawili."

📖 Sahih al-Tirmidhi, Juzuu 4, Hadithi Na. 2223:

"Baada yangu kutakuwa na Makhalifa (Viongozi) kumi na wawili."
(Al-Tirmidhi ameiweka hadithi hii chini ya mlango wa ‘Fadhail al-Khulafa’)


Mafundisho ya Sheikh Chande kuhusu Maimamu Kumi na Wawili (a.s)

Sheikh Chande alieleza kuwa Maimamu hawa si viongozi wa kawaida, bali ni watu walioteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Makhalifa na Viongozi wa Ummah huu baada ya Mtume Muhammad (saww). Akiwataja kwa majina yao mmoja baada ya mwingine, alisema kwamba Makhalifa hao kumi na wawili kwa Mujibu wa Hadithi sahihi za Mtume (s.a.w.w) ni hawa wafuatao:

  1. Imam Ali bin Abi Talib (a.s).
  2. Imam Hasan al-Mujtaba (a.s).
  3. Imam Hussein (a.s).
  4. Imam Ali Zainul Abidin (a.s).
  5. Imam Muhammad al-Baqir (a.s).
  6. Imam Ja’far al-Sadiq (a.s).
  7. Imam Musa al-Kadhim (a.s).
  8. Imam Ali al-Ridha (a.s).
  9. Imam Muhammad al-Taqi (a.s).
  10. Imam Ali al-Hadi (a.s).
  11. Imam Hasan al-Askari (a.s).
  12. Imam Muhammad al-Mahdi (a..t.f.s), ambaye yupo Ghaibuni na atarejea (atadhihiri) kwa idhini ya Allah (swt).

Hitimisho

Sheikh Chande alitoa wito kwa Waislamu wote kutafakari kwa kina mafundisho ya Mtume (saww) na kuchunguza kwa bidii vyanzo vyao wenyewe. Alisema kuwa kukubali ukweli wa Ahlul-Bayt (a.s) hakuhitaji mtu kuwa Shia, bali kunahitaji moyo wa utafiti wa haki na uadilifu wa kielimu.

Sheikh Chande alihitimisha Hotuba yake kwa kuashiria katika nukta hizi mbili na muhimu kama ifuatavyo:

·  1- Uhakika wa Hadithi hizi

  • Sheikh alionyesha kuwa wanazuoni wa Kisunni wengi wamezikubali Hadithi hizi kuwa ni Hadithi sahihi.
  • Alitoa mifano ya maelezo ya wanazuoni wa Kisunni na wanaokubali katika usunni, wanaozikubali Hadithi hii kuwa ni sahihi, wanazuoni hao ni kama vile: Ibn Hajar, al-Qunduzi al-Hanafi, na al-Suyuti.

·  2- Lengo la Mazungumzo Haya

  • Kuleta maelewano baina ya Madhehebu za Kiislamu.
  • Kuonyesha kuwa msingi wa Uimamu na Ukhalifa wa Maimam Kumi na Wawili wa Ahlul-Bayt (a.s), wanaofuatwa na Waislamu wa Madhehebu ya Shia Ithna Ashari, una mizizi pia katika vyanzo vinavyokubalika vya Kisunni.

Majlis hii ilihitimishwa kwa kisomo cha Maulid, Kaswida na Dua kwa ajili ya kuomba Baraka na muongozo wa Maimamu wa Ahlul-Bayt Rasulillah (amani iwe juu yao).

Majlis ya Mazazi ya Imam Ridha (as) yafanyika Jamiat Al-Mustafa(s), Tanzania | Hadithi Toka Vyanzo vya Kisunni Zinathibitisha Makhalifa Kumi na Wawili

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha